Baraza la Mawaziri jipya lililotangazwa jana na Rais Jakaya Kikwete lina jumla ya mawaziri na manaibu 47, wakiwemo wanawake 12, tofauti na lililovunjwa ambalo lilikuwa na idadi ya mawaziri na manaibu 60. Kati ya Mawaziri na Manaibu 60 wa Baraza lililopita 15 walikuwa wanawake na katika Baraza jipya wanawake wanne wameenguliwa na mmoja alifariki.
Aidha, jumla ya mawaziri tisa na manaibu wanane waliokuwa katika baraza lililopita wameenguliwa katika baraza la sasa. Katika Baraza hilo jipya, mawaziri wako 26 na manaibu 21 ambapo sita kati yao hawakuwepo kwenye baraza lililopita. Sura mpya katika baraza la sasa ni pamoja na Bi. Lucy Nkya, Dk. James Wanyancha, Hamisi Kagasheki, Adam Malima, Ezekiel Maige na George Mkuchika.
Halikadhalika, baadhi ya waliokuwa manaibu waziri, sasa wamepewa wizara kamili. Hawa pamoja na wizara zao za zamani kwenye mabano ni William Ngeleja (Wizara ya Nishati na Madini), Mustapha Mkullo (Fedha), Shamsa Mwangunga (Maji), Lawrence Masha (Mambo ya Ndani), Mathias Chikawe (Katiba na Sehria na Diodorus Kamala (Ushirikiano wa Afrika Mashariki).
Baraza zima la sasa ni kama ifuatavyo: Waziri wa Nchi (Utawala Bora) ni Bi. Sophia Simba wakati Waziri wa Nchi (Menejimenti ya Utumishi wa Umma) ni Bi. Hawa Ghasia. Wizara nyingine ambazo ziko chini ya Ofisi ya Makamu wa Rais ni ile ya Muungano ambayo Waziri wake ni Bw. Mohammed Seif Khatib na ya Mazingira inayoongozwa na Dk. Batilda Buriani. Kwa upande wa Wizara zilizo chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Uratibu na Bunge inaongozwa na Bw. Philip Marmo wakati ile ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Waziri wake ni Bw. Steven Wasira na Naibu ni Bi. Celina Kombani. Wizara ya Mipango na Fedha Waziri ni Bw. Mustapha Mkulo na manaibu wake ni Bw. Jeremiah Sumari na Bw. Omar Yusuph Mzee. Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii imebakia na Mawaziri wake wale wale, Profesa David Mwakyusa na Naibu wake, Dk. Aisha Kigoda wakati Wizara ya Ardhi na Maendeleo ya Makazi sasa Waziri wake John Chiligati. Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi itakuwa chini ya Waziri Profesa Jamanne Maghembe na Manaibu wake Bi. Gaudentia Kabaka na Bi. Mwantumu Mahiza.
Dk. Shukuru Kawambwa ni Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia na Naibu wake ni Dk. Maua Daftari wakati Wizara ya Miundombinu itabaki kama ilivyokuwa, yaani Waziri Andrew Chenge na Naibu Dk. Makongoro Mahanga. Kwa upande wa Wizara ya Habari, Utamaduni na Michezo, Waziri wake sasa ni Kapteni George Mkuchika na Naibu wake ni Bw. Joel Bendera wakati Wizara ya Kazi, Ajira na Maendeleo ya Vijana Waziri atakuwa Profesa Juma Kapuya na Naibu Bw. Hezekiah Chibulunje. Wizara ya Maji na Umwagiliaji itaongozwa na Profesa Mark Mwandosya na Naibu ni Bw. Christopher Chizza wakati Wizara ya Kilimo, Chakula na Ushirika Waziri ni Profesa Peter Msola na Naibu ni Dk. Mathayo David. Aidha Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto itakuwa chini ya Waziri Bi. Margaret Sitta na Naibu Dk. Lucy Nkya wakati ile ya Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi Waziri ni Bw. John Magufuli akisaidiwa na Dk. James Wanyancha. Wizara ya Maliasili na Utalii itaongozwa na Bi. Shamsha Mwangunga na Naibu wake ni Bw. Ezekiel Maiga. Wizara ya Mambo ya Ndani waziri wake sasa ni Bw. Lawrence Masha na Naibu wake ni Balozi Khamis Kagasheki wakati Waziri Bernard Membe na Naibu wake Balozi Seif Idd wanaendelea kuongoza Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa.
Wizara ya Nishati na Madini itakuwa chini ya Waziri William Ngeleja na Naibu ni Bw. Adam Malima. Wizara ya Katiba na Sheria itaongozwa Waziri Mathias Chikawe, Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa itaongozwa na Dk. Hussein Mwinyi na kusaidiwa na Dk. Emmanuel Nchimbi. Kwa upande wa Wizara ya Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dk. Diodorus Kamala anakuwa Waziri na Naibu wake ni Bw. Mohamed Abood Mohamed wakati Wizara ya Viwanda, Biashara na Masoko itaongozwa na Waziri Dk. Mary Nagu na Naibu wake akiwa Dk. Cyril Chami. Aidha Mawaziri walioenguliwa na wizara zao kwenye mabano ni Bi. Zakhia Meghji (Fedha), Dk. Harith Mwapachu (Usalama wa Raia), Bw. Bazil Mramba (Viwanda, Biashara na Masoko). Wengine ni Bw. Joseph Mungai (Mambo ya Ndani), Dk. Juma Ngasongwa (Mipango, Uchumi na Uwezeshaji), Bw. Kingunge Ngombale Mwiru (Siasa na Mahusiano ya Jamii) na Bw. Anthony Diallo (Maendeleo ya Mifugo). Mawaziri wengine ni Dk. Ibrahim Msabaha (Ushirikiano wa Afrika Mashariki) na Bw. Nazir Karamagi (Nishati na Madini). Manaibu Mawaziri walioenguliwa na wizara walizokuwa wakiongoza kwenye mabano ni Bw. Abdisalim Khatib (Fedha), Bi. Zabein Mhita (Maliasili na Utalii), Bi. Ritha Mlaki (Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi), Bw. Luka Siyame (Ofisi ya Waziri Mkuu), Bw. Ludovick Mwananzila (Elimu na Maunzo ya Ufundi). Wengine ni Bw. Daniel Nsanzugwanko (Habari, Utamaduni na Michezo), Bw. Gaudence Kayombo (Mipango, Uchumi na Uwezeshaji) na Bw. Charles Mlingwa (Mifugo). Wakati huo huo, Rais Jakaya Kikwete amesema katika kipindi cha miaka miwili ya serikali ya awamu ya nne walikuwa wakitazama muundo wa serikali na hivyo sasa amelazimika kupunguza ukubwa wa serikali kulingana na mahitaji ya wakati uliopo. Aliyasema hayo wakati akitangaza Baraza jipya la Mawaziri mjini Dodoma jana. Alisema ukubwa wa Baraza la Mawaziri uliokuwepo ulikuwa na lengo la kugawanya majukumu kwamba kila waziri afanye kazi katika eneo dogo, na baada ya kuona majukumu hayo yametekelezeka ipasavyo, sasa ameamua kupunguza idadi ya mawaziri. Rais alisema baada ya kupita miaka miwili ya serikali ya awamu ya nne walilazimika kufanya tathmini na baadaye kuona umuhimu wa kupunguza na kuunganisha baadhi ya wizara. Wizara pekee iliyoondolewa ni ya Siasa na Uhusiano wa Jamii, iliyokuwa ikiongozwa na Bw. Kingunge Ngomale-Mwiru na kwamba shughuli za wizara hiyo zitakuwa chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu. Aidha Wizara ya Mipango, Uchumi na Uwezeshaji na Fedha zimeunganishwa na kuwa moja wakati Tume ya Mipango itaundwa upya ili kiwe chombo kikuu cha serikali na kitakuwa chini ya Ofisi ya Rais. Wizara ya Mambo ya Ndani na ile ya Usalama wa Raia, nazo zimerudi kama awali na kuwa wizara moja. Wizara ya Elimu ya Juu, Sayansi na Teknolojia na ile ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, alisema zinaunganishwa na kuwa wizara moja. Hata hivyo, alisema kutokana na ongezeko la shule za sekondari za kata, elimu ya sekondari na ya msingi zitasimamiwa na Wizara ya Nchi Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI). Kwa mujibu wa Rais Kikwete, masuala yote yanayohusisna na elimu, akimaanisha kuanzia ile ya awali, yatakuwa kwenye wizara moja. Aidha alisema, masuala yote yanayohusu Sayansi, Taknolojia kwa maana mawasiliano, posta, simu, teknolojia ya habari na mawasiliano, nazo zitakuwa kwenye wizara moja. Rais alisema, Kamati ya Usimamizi ya Pamoja ya kushughulikia masuala ya Muungano, yatakuwa chini ya Ofisi ya Makamu wa Rais na kwamba ndiye atakayekuwa mwenyekiti wa vikao vya mazungumzo ya Muungano.
Kuhusu Idara ya Umwagiliaji iliyokuwa Wizara ya Kilimo, Chakula na Ushirika sasa shughuli hizo zitahamia wizara ya Maji, wakati uvuvi iliyokuwa Wizara ya Maliasili na Utalii, sasa shughuli zake zinahamishiwa Wizara ya Mifugo. Kwa upande wa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, alisema Katibu Mkuu wa Wizara ya Sheria na Katiba ndiye alikuwa Naibu Mwanasheria Mkuu, lakini sasa Katibu Mkuu wa wizara hiyo atakuwa mtu tofauti ili abaki na jukumu la utawala.
SOURCE: Nipashe 13/02/2008
SOURCE: Nipashe 13/02/2008
No comments:
Post a Comment