Kumbe ni Dili! 2008-03-04 16:35:15 Na Emmanuel Lengwa, Jijini
Wakati ni jana tu moto ambao chanzo chake hakijafahamika, uliunguza sehemu kubwa ya chini ya jengo la Ushirika lililopo mtaa wa Lumumba na kusababisha hasara ya mamilioni ya pesa, kuna madai kuwa hilo ni dili la mafisadi waliokuwa wakijaribu kuhujumu taarifa na nyaraka muhumu zilizo kwenye moja ya ofisi nyeti iliyo kwenye jingo hilo. Taarifa zilizolifikia gazeti hili zinadai kuwa ofisi iliyolengwa ni ile sababu za kuwepo kwa hisia za mkono wa mafisadi katika kulichoma moto jengo hilo, zinaelezwa kuwa ni kuwepo kwa ofisi za msajili wa makampuni nchini katika jengo hilo, BRELA, ambazo zimehifadhi data za makampuni yote yakiwemo yale tata ya Richmond, Kagoda, Meremeta na mengineyo. Wakizungumza na Alasiri, baadhi ya watu wameonyesha wasiwasi wao huo kwa kudai kuwa, mafisadi wana mbinu nyingi na hivyo wanaweza kuwa ndio waliocheza dili la kuchoma moto jengo hilo kwa nia ya kuteketeza taarifa nyeti zilizopo humo. ``Sidhani kama moto huu ni wa bahati mbaya... naamini mafisadi wamejaribu kutia mkono, ingawa wameshindwa kutimiza azma yao,`` amesema Bw. James Changalawe, mkazi wa Tandika. Mkazi mwingine wa Mwenge Bi. Judith James amesema kuungua kwa jengo hilo lenye ofisi za BRELA kunaleta wasiwasi mkubwa. ``Ule moto unaweza kuwa ni ajali kama inavyoonekana katika taarifa za awali toka polisi... lakini ieleweke kuwa mafisadi wana mbinu nyingi katika kufanikisha yale wanayoyataka,`` akadai Bi. Judith. Aidha, akizungumza na Alasiri leo asubuhi, Katibu Mkuu wa CHADEMA, Dk. Wilbroad Slaa, amesema mafisadi wanaweza kufanya balaa hilo la kutaka kuunguza ofisi za BRELA kutokana na ukweli kuwa hivi sasa, wanahaha kufuta kila aina ya ushahidi unaoweza kuwatia hatiani. Akielezea zaidi, Dk. Slaa ambaye amekuwa mstari wa mbele katika kuibua vitendo vya ufisadi wa kutisha vinavyozorotesha jitihada za Serikali katika kuwaletea maisha bora wananchi, amesema ukimya wa Serikali katika tuhuma nyingi zilizopo ni baadhi ya sababu ambazo hata sasa anaamini kuwa zinawapa mafisadi mwanya wa kuweza kufanya mbinu chafu za kupoteza ushahidi, ikiwemo kama hiyo ya hisia za kuchoma moto jengo lililo na ofisi za BRELA. Dk. Slaa amesema kutokana na maswali mengi yaliyokosa majibu Serikalini, matukio yote haya hayawezi kuacha kuhusishwa na ufisadi. Akielezea baadhi ya masuala ambayo Serikali haijayatolea maelezo, Dk. Slaa amesema katika ripoti ya Kamati Teule ya Bunge ya kuchunguza mkataba wa Richmond, ilielezwa kuwa kuna afisa mmoja wa BRELA aliyejengewa nyumba Chang`ombe na kuwekewa fanicha baada ya kufanikisha wizi wa nyaraka. Akasema suala hilo bado Serikali haijalitolea maelezo na huenda likawa limechangia jengo hilo kuchomwa moto na mafisadi. Pia Dk. Slaa amesema kitendo cha Serikali kutotaja majina ya makampuni yanayorejesha fedha za BoT pia kinaleta wasiwasi kuwa huenda makampuni hayo yaliyosajiliwa na data zao kuwepo katika ofisi za BRELA, yamefanya mbinu za kufuta ushahidi kabla hayajaanikwa wazi. Hata hivyo bosi wa BRELA, Esteriano Mahingila amekaririwa akipuuza kuhusishwa kwa moto huo na hujuma.
SOURCE: Alasiri
Tuesday, March 4, 2008
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment